John alikuwa mtu wa watu. Kwa sababu ya mafanikio yake ya kikazi na pesa, alijikuta akitengeneza marafiki wengi na wa aina mbalimbali. Hakuwa mchoyo na mara zote alisaidia ndugu zake, jamaa zake na hata marafiki zake. Kwa sababu ya roho yake kuonekana imejaa upendo na wema wengi walimwita mtu wa watu na walimsifia kuwa na roho nzuri, roho nyeupe, damu ya kupendwa na kwamba alikuwa na nyota njema.
Siku moja John alipata matatizo kazini. Ndugu, jamaa na marafiki walipopata habari za John walisikitika sana na kupiga simu kumpa pole. John alijisikia faraja sana na moyoni alihisi kupafa afueni. Alimshukuru Mungu na kujisemea moyoni kwamba kweli haya ndiyo matunda ya utu wema. Akamshukuru Mungu kwamba wema wake haujamtupa na kwamba ametengeneza marafiki wa kweli, marafiki wa shida na raha. Akafurahi kwamba pesa zake aliwekeza pazuri kwani aliona dhahiri mtaji wake ni watu. Hivyo John hakuwa na wasiwasi wowote juu ya matatizo yaliyompata. Na hata alipofunguliwa kesi mahakamani hakuwa na wasiwasi kwani moyoni alijua anao marafiki wa kumtetea. Marafiki aliokaa nao pamoja, kula kunywa pamoja na hata kubadilishana mawazo pamoja
Kesi yake ilipokaribia, John alianza kuwatafuta marafiki zake wapendwa ili wamsaidie kutoa ushahidi wa utetezi wake mahakamani. Akachukua simu yake iliyojaa marafiki wa kila aina na kumpigia rafiki wake wa kwanza, swahiba ambaye walikuwa karibu sana miaka yote na hakuna siku hata moja iliyopita pasipo kuwa pamoja. Wakakubaliana kukutana na kama ilivyoada walikutana masaa machache baadaye. John akatumia fursa hiyo kumsimulia rafiki yake kuhusu maendeleo ya kesi yake na kumuomba kufika mahakamini ili awe shahidi katika kesi inayomkabili.
John alipigwa na butwaa pale alipoambiwa na rafiki yake kwamba hawezi kamwe kwenda mahakamani kutoa utetezi juu yake. “Wewe ni rafiki yangu wa dhati, lakini kwa hili utanisamehe, kwa kweli siwezi katakata kusimama mahakamani kwa ajili yako. Kumbuka John nina watoto na familia na haya mambo yako ni magumu, wewe pambana tu mimi niko pamoja nawe” John aliishiwa nguvu na kubaki mdomo wazi kwani hili ni jibu ambalo hakulitegemea kutoka kwa swahiba wake huyu
John hakuongea maneno mengi na huku ameinamisha kichwa chake chini aliondoka kimyakimya kuelekea nyumbani. Alipofika nyumbani aliwaza na kuwazua na kisha akapiga moyo konde kumtafuta rafiki wake wa pili. Huyu hawakuwa naye karibu kama wa kwanza lakini walipenda kukutana pamoja siku za mwisho wa wiki ili kupata moja moto moja baridi pamoja na kutizama mpira. Kwa kuwa hakuwa na nguvu za kutembea kutokana na jibu la swahiba wake, aliona aeleze jambo lake kwenye simu. Rafiki yake kwa masikitiko makubwa alisema “rafiki yangu John, pole sana kwa matatizo yaliyokupata, hii dunia ndivyo ilivyo lakini Mungu mkubwa utashinda. Mimi nitakusindikiza mpaka mahakamani, lakini sitoweza kuingia ndani ili kukutetea. Kwa kweli katika maisha yangu sijawahi hata siku moja kuitwa kituo cha polisi, sasa huko mahakamani nahisi ndio balaa tupu!niambie tu saa ngapi nikupitie nikusindikize lakini tafadhali usinielewe vibaya”
John kusikia maneno haya alizidi kukata tamaa na kuhisi tayari yuko gerezani. Matarajio yake yote yalianza kufifia kama jua linalozama na kuhisi dunia imemchapa bakora. Akakumbuka wema wake wote aliowatendea marafiki zake na akashindwa kuamini kinachotokea. Akahisi Mungu amempa kisogo na kutamani dunia ipasuke ili aingie. Lakini baadaye akakumbuka kwamba anaye rafiki mwingine ambaye huwa hawaonani mara kwa mara lakini mara moja moja ndani ya mwezi huwa wanapishana barabarani na kukutana kanisani au kwenye misiba. Kwa sababu hakuwa na jinsi ya kufanya, na kwa sababu hakuwa hata na namba yake ya simu aliamua kwenda kumuulizia kanisani na kupata namba yake ya simu. Alimpigia akimuomba wakutane mara moja popote alipo. Yule rafiki wa tatu alishtuka sana kwani haikuwa desturi kwa John kumtafuta kwa udi na uvumba namna ile. Akamwambia “usijali John kwani wewe uko wapi? Mimi nitakufuata popote ulipo” John akashukuru na kumuomba afanye hivyo.
Baada ya kukutana, John alimuelezea matatizo aliyo nayo. Alifanya hivyo ili kutimiza aja ya moyo wake tu kwani hakuwa na tegemeo lolote la kupata msaada. Kwanza hawakuwa karibu, pili pamoja na mafanikio yake hakuwahi kumkumbuka rafiki yake huyo kwa nama yoyote ile. Lakini kwa mshangao mkubwa rafiki yake huyo alimkubalia John na kumtia moyo akimwambia mimi sitokuacha uangamie. Pamoja na kwamba siko karibu na wewe, nimekuwa nikikufuatilia kwa karibu na ninaujua ukweli wa matatizo yako. Nitasimamia kweli na hiyo kweli itakuweka huru.
Kesi ya John iliunguruma na baada ya muda kupita hakimu alitoa uamuzi.John alikutwa hana hatia na ikatangazwa rasmi kuwa John yuko huru na kwamba anaweza kuendelea na kazi na maisha yake ya kila siku kama kawaida. John hakuwa na namna ya kumshukuru rafiki yake zaidi ya kumshukuru Mungu. John akaanza kurudisha ufahamu na kutafakari maisha yake kwa kina ikiwa ni pamoja na marafiki, ndugu na jamaa waliomzunguka. Akagundua kwamba kila rafiki yake ana kiwango anachoweza kumsaidia. Ya kwamba ni rafiki mmoja tu aliyekuwa tayari kujitoa mhanga kwa sababu yake.
maisha ya John yanatufundisha nini?Mimi na wewe leo hii tuna marafiki wengi walio katika makundi matatu kama marafiki wa John. Rafiki wa kwanza ambaye ni PESA na mali, rafiki wa pili ambaye ni MARAFIKI, NDUGU NA JAMAA na rafiki wa tatu ambaye ni MUNGU.
Kuna mambo makubwa mbayo marafiki, ndugu, jamaa, mke au mume wako watakufanyia kwa upendo wa hali ya juu. Lakini kuna mambo na nyakati ambazo ni rafiki mmoja tu anayeweza kukutetea na rafiki huyo ni rafiki wa tatu yaani Mungu. Hata itakapofika siku yetu ya mwisho, siku ya kutangulia mbele za haki, pesa na magari na nyumba havitokubali kwenda na sisi mahakamani. Vitatuonea huruma lakini vitatuacha twende peke yetu bila kujali gharama tuliyowekeza kwao.Rafiki wa pili; ndugu, jamaa na marafiki kwa upendo kabisa watakusindikiza mpaka makazi yako ya mwisho kama alivyofanya rafiki wa pili wa John. Lakini hawatokubali kuingia ndani ili wakutetee. Watasikitika sana lakini watabaki nje wakikukumbuka kwa huruma ukipambana mwenyewe mahakamani. Ndipo hapo utakapoona umuhimu na kumkumbuka rafiki wa tatu. Yeye ni Mungu muumba wa mbingu na ulimwengu. Huyu ni rafiki ambaye hatokubali kukuacha peke yako. Ingawa humkumbuki mara kwa mara kwa zawadi kama rafiki wa kwanza na wa pili lakini yeye hatokuacha yatima. Ataingia pamoja na wewe mahakamani na kukutetea mpaka mwisho.
Huu ndio ukweli kuhusu maisha. Kumbuka kwamba unao marafiki hawa watatu. Kila siku unakutana na kusaidiana na rafiki wa kwanza na wa pili. lakini maisha ya John yanatufundisha umuhimu wa kupata muda wa kumjali rafiki wa tatu. Kwa sababu ni yeye tu awezaye kututetea katika nyakati ambazo rafiki wa kwanza na wa pili hawatokuwa tayari kututetea hata kama wanatupenda kupita maelezo.











Discussions
marafiki watatu
Huo ndio ukweli maana ukiwa na pesa kwa jamii yetu ya kiafrica daima utakuwa na ndugu wengi, jamaa ndio usiseme, Pana msemo mmoja wanasema wagirik kuwajoki waafrika kwamba mwafrika akipata pesa ni sawa na ndege mmoja aliye angani akaachia jivi kumbe katika kile kinyesi chake palikuwamo mbegu fran ya mti mkubwa kinyesi kile kikadondoka katika jangwa pakatokea ile mbegu ikaota na ikastawi vema mwisho wa siku ukawa mti mkubwa sana katika eneo lile. Ikitokea ndege wakawa katika safari zao wote upumzika katika mti ule, hatimae ule mti UKAUKA kutokana na kuzidiwa na kinyesi na pilika za ndege wale, Maana ufikia hatua wakatafuna hata matawi, HAKIKA Huo ndio uafrica,
hakika nimeipenda hii habari mungu awabaliki .
Kamgisha.